description
2Hali halisi katika jamii zetu inaonesha kwamba kuna vilio vya aina nyingi. Haipiti siku bila kusikia watu wakilaumu, wakinung'unika, na wengine wakilia hadi kutoa machozi. Ukifuatilia nini kinasababisha vilio hivyo, utasikia sababu nyingi. Lakini sababu mama, yaani sababu ile inayotawala na pengine kuzimeza sababu nyingine zote au kusababisha hizo nyingine ziwepo ni uongozi. Nisemapo uongozi, ninamaanisha watu wale waliopo kwenye nafasi za kuhakikisha au kusimamia mambo katika jamii ili yaende sawa sawa. Maana utasikia kiongozi fulani amewaonea watu, amewapendelea hawa na kuwanyima haki wale, ametumia mali ya taasisi bila kufuata utaratibu au ametumia kwa manufaa binafsi. Na kama ndiyo ameharibika zaidi, utasikia amejinufaisha kupitia watu anaowaongoza. Kwa lugha ya kidini, utasikia amekula kondoo. Kwa sababu ya mambo haya yote, jamii nyingi zimejawa na watu wenye makovu na majeraha yanayosababishwa na uongozi. Hivi ni kwa nini uongozi uliowekwa ili uisaidie jamii, badala ya kufanya hivyo, unaijeruhi jamii? Mwandishi wa kitabu hiki anajadili kuwa sababu kuu ya kiongozi (mtumishi) kusababisha maafa katika jamii anayoitumikia ni kukosekana kwa uchaji katika maisha yake. Maana mtumishi akishindwa kuwa mchaji atafanya makosa. Bila kujali ngazi yake yake, kosa la kiongozi lina harufu tofauti na makosa ya watu wa kawaida. Kwa hiyo, kwa njia ya kitabu hiki, mwandishi anatoa wito kwa watumishi na viongozi wa aina zote kujifunza maisha ya uchaji. Mwandishi anaonesha namna jamii inavyoweza kufaidika pale kiongozi au mtumishi anapokuwa mcha Mungu.